Kipindi mafunzo yamekolea na askari hao wakiwa wameshakamilika
tayari kwa utekelezaji wa mauaji hayo, lilitolewa agizo la Serikali kuwa mpango
wa Kikosi 684 umefutwa.
Sababu ya kufutwa mpango huo ni kufuatia maelewano ya
kidiplomasia kati ya Korea Kusini na Kaskazini kufikia hatua nzuri. Kipindi
hicho Kikosi 684 kilikuwa bado kipo Silmido.
Agosti
23, 1971, makomando wa Kikosi 684 waliua walinzi wao pamoja na wahudumu,
wakavuka Bahari ya Njano (Yellow Sea), wakateka basi na kupanda kuelekea mji
mkuu wa Korea Kusini, Seoul.
Safari yao ikawa kuelekea Ikulu ya Korea Kusini, Blue House ili
kumuua aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Park Chung-hee.
Vikosi vya Jeshi la Korea, vilikizingira Kikosi 684, katika eneo
la Daebang-dong, Dongjack-gu, Seoul. Askari 20 wa Kikosi 684 waliuawa na
wengine kujiua eneo la tukio, wanne waliobaki walihukumiwa kifo na walinyongwa
Machi 10, 1972.
Mpaka leo swali limebaki ni sababu gani Kikosi 684 walitaka
kumuua Rais Chung-hee? Huo ndiyo uasi wa kijeshi ambao haujawahi kubainika
sababu yake.
MATOKEO
Serikali ya Korea Kusini ilinyamaza, haikutoa taarifa yoyote
kuhusu makomando wa Kikosi 684.
Mwaka 2006, Korea Kusini iliamua kuvunja mzizi wa fitina kwa
kueleza bayana kilichotokea kuhusu Kikosi 684.
Baada ya taarifa hiyo, familia za makomando wa Kikosi 684
waliipeleka Serikali mahakamani na kushinda kesi.
Serikali iliagizwa kuzilipa fidia familia za makomando wa Kikosi
684 kwa sababu makomando hao walipewa mafunzo makali bila tahadhari yoyote.
Walivurugikiwa akili na kujaribu kufanya shambulio. Serikali badala ya
kuwaelewa kuwa hawakuwa sawa, wakawachukulia kama waasi.
NINI UNAPATA?
Korea Kusini waliingia gharama kubwa zaidi walipojaribu kulipa
kisasi. Walipoteza makomando wote 31. Chupuchupu Rais wao auawe. Zaidi,
waliingia gharama ya kuendesha kesi na kunyonga kisha kulipa fidia familia za
marehemu wote 31.
Adui yako akishindwa mpango wake mbaya juu yako, shukuru Mungu
ambaye amekunusuru. Usijione umemzuia kwa nguvu na maarifa yako.
Ukijiona jabali na kupanga kulipa kisasi, unakuwa unamkosea
Mungu aliyekulinda.
No comments:
Post a Comment