Halipo jambo baya ambalo unaweza kumfanyia mwenzako kisha isiwezekane wewe
kufanyiwa. Hayapo maumivu ambayo mtu anaweza kumsababishia mwenzake halafu
kusiwe na uwezekano wa yeye kuumizwa kwa namna ileile.
Sayansi ya Sir Isaac Newton inatwambia: “For every action, there is an
equal and opposite reaction.” Kwamba: Katika kila tendo, kuna matokeo kusudiwa
au matokeo yaliyo kinyume.
Kama
siku zote utaishi ukifahamu kuwa baya unaloweza kumfanyia mwenzako na wewe
inawezekana kufanyiwa, utakuwa umepata kinga bora ya maisha. Kinga hiyo
ukamilifu wake ni kujiuliza maneno matatu; Kama Ingekuwa Mimi
Unaelekea kutenda dhambi na mume au mke wa mwenzio, jiulize
ingekuwa mkeo au mumeo ndiye anakwenda kutenda dhambi hiyo ungefurahi? Tendo
lako linakwenda kuumiza watu wawili; mwenzi wako na yule unayemuibia.
Unamsemea uongo mfanyakazi mwenzako kazini ili afukuzwe kazi na
kweli unafanikiwa. Usifanye uchonganishi huo kabla hujajiuliza; ingekuwa wewe
ndiye unachongewa kazini na kufukuzwa ungejisikiaje
Waza kabla hujatenda ubaya; Kama Ingekuwa Mimi! Meneno hayo
yatakujengea kumbukumbu kuwa upo ubaya wenye uelekeo uliokusudia, vilevile upo
ubaya wenye uelekeo wa kinyume.
Kwamba ukimrubuni mume au mke wa mwenzio ili utende naye dhambi,
vivyo hivyo inawezekana mwenzio naye akamrubuni mumeo au mkeo akatenda naye
dhambi. Jiulize; ingekuwa wewe ungeumia kiasi gani?
Mkeo au mumeo anakulalamikia kuhusu aina ya maisha yako, kwamba
yanatoa kipaumbele kwa watu wengine kuliko yeye mwenzi wako. Pengine yanamfanya
awe na wasiwasi juu ya uaminifu wako. Wewe unampuuza kisha uanaendelea na tabia
hizohizo. Waza; Kama Ingekuwa Mimi!
Kama Ingekuwa Mimi ni maneno ambayo ingependeza kila mmoja
ayaweke kichwani na ayaishi. Yakitumika vizuri kwa kila mmoja hujenga mapatano
yenye nguvu na afya kwenye jamii. Huyeyusha madonge ya chuki na visasi. Hujenga
utulivu wa kijamii, kuheshimiana na kuhurumiana.
Daktari awaze ingekuwa ndiye yeye anakataa kumtibu mgonjwa mpaka
apewe rushwa. Jaji au hakimu ajiulize kama angekuwa ndiye yeye mtu mnyonge
anayehukumiwa kwa ushawishi wa rushwa. Polisi ajiulize kama ndiye yeye angekuwa
anabambikiwa kesi.
No comments:
Post a Comment