Kwa kawaida uamuzi wa kujenga taifa lenye watu wa aina fulani u
mikononi mwa wananchi wenyewe na wananchi ni mimi na wewe. Kwa hiyo mchango
wako wewe na mwingine na mwingine (uwe hasi au chanya) unachangia kujenga jamii
ya aina fulani na hatimae taifa la aina fulani.
Kwa kawaida jambo lolote liwe jema au baya, huanza kama fikra,
hutolewa kama hoja, huchambuliwa na kisha hutekelezwa ili kuleta matokeo ya
aina fulani.Kitendo cha mtu kuamua kutojilazimisha
kufikiri vya kutosha, humfanya asiwe na mawazo yenye mtiririko mzuri ndani ya
kichwa chake , kitu kinachomfanya anapoongea ashindwe kutoa hoja na ajikute
akipiga kelele tu ambazo kimsingi hazina athari yeyote ya maana katika jamii.
Kasi
ya wengi wetu kupiga kelele badala ya kujibu hoja pale tunapoulizwa ni kwanini
vyama vyetu havijafanya jambo fulani ambalo vilitakiwa vilifanye, au kwa nini
vimefanya jambo fulani kinyume na ilivyotakiwa kufanya au kwani nini vimefanya
jambo ambalo halikutakiwa kufanywa kabisa, imeongezeka sana!.
Inavyoonekana tatizo hili kwa kiwango kikubwa huchangiwa na
wengi wetu kuamua kutochambua mambo tunayoyaona, kuyasikia au kuyasoma amma kwa
makusudi, kwa kusikiliza ya kuambiwa tu badala ya kuchanganya na zetu, au kwa
kukosa uwezo (ni jambo la mjadala), au kwa uzembe.Ni kitu cha kawaida sana siku
hizi chama, mwanachama au kiongozi anapoulizwa swali, badala ya kujibu swali
huibuka na kuanza kupiga kelele.Mara utasikia mnafiki wewe! msaliti wewe,!
mburura, kachukue hela yako! wewe mwanamke au mwanaume n.k.
Kwa kuwa taifa hujengwa na wewe na mimi, na kwa kuwa mazoea
hujenga tabia; basi ni hiari yetu kuchagua kujenga Taifa la wapiga kelele! kwa
kujizoeza kupiga kelele mbele ya hoja au taifa la wajenga hoja kwa kujizoeza
kukabiliana na hoja zinapojitokeza.
Wanasema dunia ni yetu chaguo ni letu na akili kumkichwa.
No comments:
Post a Comment