Unahitaji kuwa na uhakika kuhusu Usalama wa watoto; je, mwenzi
wako ataweza kuhakikisha mtoto au watoto mtakaowapata wanakuwa salama?
Usipuuze eneo hili. Unatakiwa kuwa na mpenzi ambaye anatambua
wajibu wake kama baba au mama kwa watoto. Vinginevyo huyo mwenzi wako uwe huna
mpango wa kuzaa naye.
Kwa
wapenzi wenye dira ya maisha, mwanzo wa uhusiano wao humaanisha hatua muhimu
kuelekea kujenga familia. Hapohapo unapaswa kufahamu kuwa familia ni watoto.
Kama ni mtu mwelewa basi unatakiwa kufahamu kuwa watoto ni
zawadi kubwa zaidi ambayo binadamu hupewa na Mungu. Hivyo, kuwalea vizuri na kuwapa
huduma bora ni jambo la lazima na lenye kuhitaji umakini wa hali ya juu.
Hivyo basi, kama unafikiria Usalama wa mtoto au watoto wako,
unapaswa kujua ni aina gani ya mtu ambaye unaingia naye kwenye mapenzi. Je,
ukiwa naye kisha mkapata watoto, watakuwa salama?
Usije kuvamia mtu ambaye ugomvi kidogo yeye anakukimbia na
watoto hawataki tena. Mgombane ninyi, adhabu waipate mpaka watoto wasio na
hatia. Mwingine anatoroka na watoto bila kufahamu kuwa mtoto anahitaji mapenzi
ya wazazi wote wawili.
Wapo wale ambao sura ya binadamu roho ya chatu, mnagombana ninyi
kwa sababu za kimapenzi, yeye anakwenda kuchinja au kuwapa sumu watoto, akiona
kufanya hivyo ndiyo uamuzi sahihi.
Watu wengi wanapoyafikiria mapenzi yao huongozwa na ubinafsi.
Hujifikiria wao wenyewe, huwa hawawawazii watoto ambao kesho watakuja na
kuhitaji malezi bora yenye ushirikiano mzuri kati ya baba na mama.
Hili pia watu wanatakiwa kufahamu kuwa hakuna zawadi kubwa kwa
mzazi kwenda kwa mtoto au watoto wake, kama kumhakikishia mapenzi na uangalizi
wa macho ya wazazi wake wote wawili.
Je, tayari una mtoto na unafikiria kuingia kwenye uhusiano na
mtu mwingine tofauti na yule uliyezaa naye? Kama ndivyo kanuni ni hiyo,
usijifirie wewe, mtazame huyo unayetaka kuingia naye kwenye uhusiano, je,
anatambua mwanao ni mwanaye?
Jilinde siku zote usije kumpa mateso mtoto wako kwa kuangukia
kwa mtu ambaye hatambui thamani ya kuwa mzazi. Hii iwe kanuni yako na
ujiridhishe kuwa ukiwa naye, Usalama wa mwanao utakuwa wa uhakika.
No comments:
Post a Comment