Unapopata mpenzi au tayari unamtambua kama mwenzi wa maisha yako
kwa sababu tayari mpo kwenye ndoa, unapaswa kuzingatia kuwa binadamu wana
historia tofauti za kimaisha.
Huyo mwenzi wako anaweza kuwa anatabasamu na wewe leo, lakini
kabla ya kukutana na wewe, ametoka kulia machozi mengi mno. Baada ya kukutana
na wewe anakuona faraja na kifutio cha machozi yake yote ya nyuma.
Unaweza
usiwe ndani yake kujua ni kwa kiasi gani alikata tamaa ya maisha kabla ya
kukutana na wewe. Hata hivyo, baada ya kukupata, ghafla anajiona yupo kwenye
ulimwengu mpya wenye raha zenye kumsahaulisha kumbukumbu mbaya alizopitia.
Nakwambia huwezi kujua baada ya kukupata umemfanya ajae
matumaini ya kiasi gani. Na huwezi kutambua ni kwa thamani kubwa kiasi gani
anakuthamani baada ya yote magumu aliyopitia kabla yako.
Kwa vile huishi kwenye fikra zake hutaweza kutambua ni kwa kiasi
gani wewe ndiye mantiki ya dunia yake. Jinsi anavyokuhitaji ni sawasawa na
anavyoihitaji dunia. Sababu ni moja tu kwamba ametoka kwenye mengi yenye
kumtesa kabla yako.
Anakuheshimu na unaona, anakupenda na huo upendo wake unauhisi
kikamilifu. Wajibu wako unakuwa ni mmoja tu, kumpenda sawasawa na anavyokupenda
au wewe zidisha. Mpe heshima sawasawa na anavyokuheshimu au mzidishie. Ukifanya
hivyo, utamfanya azidi kuiona dunia imenyooka sana upande wake baada ya
kukupata.
Ikiwa mwenzi wako anakuona wewe ni dunia yake, maana yake wewe
pia ni kifo chake. Dunia isipokuwepo kuna maisha tena? Sasa basi, hakikisha
upepo na imani yake kubwa kwake unavitunza na unampa uhakika kuwa yupo kwenye
mapenzi salama.
Ukienda kinyume utamsababishia mauti mwenzako. Ukimtenda utamrejeshea
kumbukumbu mbaya alizodhani amezifuta. Lazima utambue nafasi yako kwenye
mapenzi na maisha yako yawe ulinzi tosha kwake.



No comments:
Post a Comment